Pages

Monday, June 6, 2016

Mwanamziki mkongwe aitwaye "Sugu" Kutoka Muziki na Maisha mpaka Siasa na Maisha

By Nemmy Kim.


Joseph Osmund Mbilinyi maarufu kama Mr Two, 2 proud au Sugu ni mkongwe katika muziki wa kizazi kipya nchini na pia ni mbunge wa Mbeya Mjini kwa awamu ya pili sasa. Kwa jinsi ambavyo Sugu anavyoipenda Mbeya unaweza kusema ndipo sehemu ambayo alizaliwa au ndio asili yake lakini ukweli ni kwamba Sugu alizaliwa mkoani Mtwara katika hospitali ya Ligula.

Sugu asili yake ni Songea mkoani Ruvuma (inawezekana akawa Mngoni) tofauti na watu wengi wanavyodhani kwamba ni Mnyakyusa. Sugu alihamia mbeya mwaka 1987 baada ya baba yake kuhamishiwa kikazi mkoani humo.
Sugu alizaliwa tarehe 01.05.1972 na ndio kisa kuitwa Mei enzi za utoto wake kwa sababu ya kuzaliwa siku ya wafanyakazi duniani (May Day). Tarehe 24.09.1992 ni siku ambayo Sugu hawezi kuisahau katika maisha yake. Ni siku ambayo Sugu alimpoteza Baba yake mzazi ambaye ndiye alikuwa tegemeo la familia katika nyanja zote za maisha. Katika siku za mwisho za uhai wa baba yake alipewa usia kwamba aitunze familia yake; hivyo kwenye kibao cha “Hayakuwa Mapenzi” aliposema “Baba alipofariki ilibidi nimtunze mama na zaidi kuhakikisha wadogo zangu wanasoma” haikuwa mistari tu alikuwa anazungumzia maisha yake halisi.
Wakati baba yake anafariki Sugu alikuwa na umri wa miaka 20. Ni wakati huo Sugu alikuwa anamalizia kozi ya “Clearing and Forwading” katika chuo cha “Equatorial Training College” kilichokuwa Dar es salaam. Wakati huo pia sugu alikuwa ameshaanza kujishughulisha na muziki.
Kwa ufupi alikuwa mwanamuziki tu hakuwa mfanyabiashara kama anavyosema na muziki wenyewe ulikuwa haulipi kwakuwa ulionekana kama uhuni. Sugu anasema hata Elimu ya “Clearing and Forwarding” aliyosoma hakuwa akiipenda bali alisoma ili apate nafasi ya kuishi Dar es salaam.
Usia aliopewa wa kuihudumia Familia ndilo suala lililomfanya mwaka 1993 awe boda akiitafuta South Africa. Hiyo ilikuwa ni mwaka mmoja baada ya kifo cha baba yake. Katikati mwa miaka ya tisini ndio wakati ambao Sugu alijikita zaidi katika masuala ya muziki kilichofuata baada ya hapo ni historia kubwa kuandikwa na ndugu Joseph Mbilinyi; Tanzania inajua na Dunia inajua (In Lowassa`s Voice).
Inawezekana Sugu akawa ndiye msanii wa kizazi kipya mwenye album nyingi. Mpaka sasa ametoa album takribani tisa. Album hizi ni kama “Ni Mimi” iliyotoka mwaka 1995, Ndani ya Bongo (1996), Niite Mr II (1998), Nje ya Bongo (1999), Millennium (2000), Muziki na Maisha (2001), Itikadi (2002), Sugu (2004), Coming of Age-Ujio Wa Umri (2006) na VETO iliyotoka mwaka 2009.
Wakati anatoa album yake iitwayo “MUZIKI NA MAISHA” mwanzoni mwa miaka ya 2000 ndio wakati alipoamini kwamba muziki ndio mkombozi wake kiuchumi ndio wakati ambao alianza kukumbwa na masaibu/changamoto zilizopelekea mpaka akaamua kutundika daluga za usanii. Changamoto hizi ambazo zilikumkumba mwanzoni mwa miaka ya 2000 mpaka 2010 ndizo zilizokuja kui-prove wrong ama kuikosoa dhana yake ya “Muziki na Maisha”. Ntaelezea changamoto hizo kama ifuatavyo.
Ni katika kipindi hiki ndipo alipoanza kupigwa vita ya kummaliza kimuziki ikiwa ni pamoja ni kupunguza kucheza kazi zake katika vyombo vya habari. Vita hivi vilitokana na yeye kuonekana mtu asiyetaka kudhulumiwa au kupoteza haki yake. Inawezekana watu hawa walikuwa hawajui kwamba sugu “amepata sana tabu maisha yake yote” ndio maana akashangaa walipoleta chuki bila sababu wakati alipopata raha kidogo.
Hii sanaa ya Tanzania haina mwenyewe; ilifikia hatua Sugu na yeye akaanza kuombwa hela na watu wa vyombo vya habari kwa ajili ya promo licha ya kuutumikia muziki kwa muda mrefu. Sugu anamtaja moja kati ya wafanyakazi wa kituo kimoja cha TV kuwa alimuomba kifuta jasho ili video ya wimbo wake wa Moto Chini iweze kupewa airtime. Ilifikia hatua akawaza kuwa aende PCB (Kwa sasa PCCB au TAKUKURU) awapelekee pesa “za moto” lakini akapata wazo la kuridhika kwamba “kama hautacheza nyimbo zake redioni haina maneno kwani hata asiporap dili zake ni milioni moja, mbili, tatu, nne mpaka tano.”
Ni wakati huu huu pia Sugu alijikuta anayalalamikia Mapenzi baada ya kutendwa na mpenziwe katika wimbo wa ‘Hayakuwa Mapenzi’ ambayo inasemekana ni stori ya kweli iliyomtokea. Hii ni baada ya kuachwa na mpenzi wake kisa wazazi wa mpenzi wake walimuona yeye (Sugu) hana future, ingawa hawapi lawama kwa kumtakia mema binti yao lakini hayo hayakuwa mapenzi halisi. Ile dhana ya Mungu anampangia kila mmoja ni dhana inayoaminiwa na wachache sana ambao mpenzi wake na wazazi wake hawakutaka kuwa kati ya watu hao wachache.
Sugu sidhani kama ataweza kusahau jinsi alivyovamiwa na majambazi na kuibiwa. Hii ilikuwa ni baada ya kurudi kutoka ughaibuni na vifaa vya muziki ambavyo alitaka kufanya uwekezaji katika tasnia husika. Ilikuwa ni usiku wa manane walipomvamia na kumpora kila kitu. Ingawa baadaye alikuja kuvipata vifaa vyake lakini kitu cha kushangaza wale majambazi waliomvamia na kutishia kumuua hawakuchukuliwa hatua yoyote mpaka wanadunda mtaani. Huu ni muendelezo wa vitendo vya rushwa na urasimu unaoendelea katika taasisi nyeti za serikali.
Hawezi pia kusahau jinsi ambavyo alidhurumiwa mradi wake wa kutokomeza Malaria. Shutuma zake za kwanza zilikwenda kwa ubalozi wa Marekani na ikulu ya Tanzania kwa kumuengua kwenye mchakato kisha zikahamia kwa kituo kimoja cha redio ambao wao walisema “hawahusiki kwa lolote kuhusu mradi huo zaidi ya kutoa wasanii, vyombo vya muziki na kusema wasihusishwe kwa lolote”. Kwa wenye kumbukumbu mradi huu ndio uliozinduliwa na Raisi Kikwete ukifahamika kama “MALARIA NO MORE.”
Mwaka 2000 Sugu aliamua kuingia katika ulingo wa siasa na kugombea ubunge katika jimbo la Mbeya mjini kwa tiketi ya Chadema na kufanikiwa kushinda. Kuingia katika siasa kulitokana na ushawishi mkubwa alioupata kutoka kwa Mh. John Mnyika. Kwa mujibu wa Zavara (2012) alisema kwamba Sugu inawezekana ndio akawa mwanahip hop wa kwanza duniani kuchaguliwa kuwa mbunge.
Huo ndio uliokuwa mwanzo wa uanasiasa wa Sugu. Ikumbukwe baada ya Ubunge alitoa kitabu kinachohusu maisha yake kutoka maisha ya mtaani mpaka Bungeni na ndicho kimenipa mwongozo wa kuandika makala hii kwa asilimia 50. Hata alipogombea ubunge tena mwaka 2015 alichaguliwa tena na kushinda kwa kura nyingi kuliko mbunge yeyote Tanzania.
Tunakubaliana mwaka 2010 ndiyo ulikuwa mwaka ambao Sugu aliingia rasmi katika siasa. Tangu mwaka 2010 mpaka ni miaka 6 sasa imepita. Ukiusikiliza huu wimbo wake mpya uitwao “Freedom” utagundua kuna mafanikio makubwa ameyapata alipoingia katika siasa ambayo yalishindikana kupatikana kwa miaka karibia ishirini ya kufanya kwake muziki. Tunaweza kukubaliana naye aliposema kwamba yale sio maisha yake yalikuwa ni mambo tu ya hela.
Katika maisha ya uanasiasa Sugu ameweza kuanza ujenzi wa Hoteli yake ya nyota tatu jijini mbeya itayoitwa Hotel Desderia. Sugu ameingia kandarasi ya ujenzi na Kampuni iitwayo Home Africa. Hela za ujenzi wa Hoteli zimepatikana baada ya kuchukua mkopo katika Benki ya CRDB. swali la msingi la kujiuliza je angekuwa msanii tu angeweza kupata mkopo huo? Je ni wasanii wangapi wanaweza kukopesheka kwa kiwango hicho cha mkopo?
Ikumbukwe wakati wa harakati za Vinega wa Anti Virus dhidi ya Clouds FM hakuna muafaka uliopatikana baina ya pande hizo mbili mpaka pale Sugu alipoizungumzia katika hotuba yake bungeni kama waziri kivuli. Serikali ndipo ilipoingilia kati na kuwasuluhisha Sugu na Ruge. Haijulikani kama Sugu alimalizana na Ruge kwa niaba ya Vinega au ni kwa ajili ya mradi wake wa Malaria. Tusisahau Roma alishasema kwamba Pesa ndio iliyomaliza ugomvi wa Ruge na Sugu. Unaanzaje kukataa Siasa imebadili maisha ya Sugu?
Katika dunia ya kibepari tuliyomo ukiwa na uhuru wa kiuchumi (Economic Freedom) una haki ya kujikubali mwenyewe. Huwezi kumshangaa Sugu akifanya hivyo. Wakati namtazama Suma G akifanya mazoezi na wanachuo katika viwanja vya Taasisi ya Ustawi wa Jamii ni wakati huo huo Sugu anaweza kuwa viwanja vya Gymkhana akicheza Gofu na V.I.P wenzake. Muda unakwenda, Maisha na Kampani pia zinabadilika.
Hivyo ni baadhi tu ya vitu ambavyo hakuvikamilisha wakati akiwa mwanamuziki lakini ameweza akiwa Mwanasiasa. Kama unawaza Sugu anataka kuwa mwanamuziki tu unakosea; mwenyewe anasema yuko mbioni kuwa mwanasiasa mkongwe.
Mafanikio yoyote yale huwa yana gharama zake. Ukiwa mwanasiasa unatakiwa ujue kuongopa na kulamba matapishi yako. Najua wengi watakuwa hawafahamu kuwa Sugu amewahi kulamba Matapishi yake pia. Katika wimbo wake uitwao “Kambarage” kuna mahali anasema “watu kama Chenge na Lowassa, siasa kwao ni mtaji wa kulimbikiza mapesa.”
Sugu alisema kwamba Lowassa analimbikiza mapesa kupitia siasa lakini Sugu huyo huyo kwenye kampeni za uchaguzi mwaka 2015 alikuwa akimkampenia Lowassa yule yule awe Rais. Hii ndio maana ya siasa wala hakuna cha ajabu.
Muda mwingine katika siasa unapaswa kuwa zaidi ya Petro aliyemkana Yesu mara tatu kwa watu watatu tofauti lakini katika siasa unapaswa muda mwingine kujikana mwenyewe zaidi ya mara tatu mbele ya mamilioni ya watanzania kama sio dunia.
Kitu ambacho Sugu alikuwa akifahamu wakati anaanza muziki mpaka wakati huo ni kwamba mafanikio huambatana na chuki na mara nyingine unaweza kugeukwa na wanaojiita marafiki. Wote tunajua mchango wa Sugu kwenye sanaa ya Afande Sele lakini jambo la kushangaza ni pale ambapo Afande Sele alikubali kufanya shoo ya Ludacris (Leaders Club) wakati ilikuwa ni shoo iliyoandaliwa siku moja na shoo ya Vinega wakiongozwa na Sugu ili kuidhoofisha shoo ya kina Sugu. Ndio maana sishangai anaposema kuwa sasa analala macho wanafiki hawataki na hatojali wanachosema.
Miaka michache iliyopita (sio mingi sana) Afande alilalamika kwamba Sugu tangu achaguliwe kuwa mbunge hajaipigania chochote sanaa. Sugu alijibu kwamba yeye sio mbunge wa wasanii yeye ni mbunge wa Mbeya mjini. Alijibu vyema lakini alitakiwa kukumbuka Mbeya Mjini kuna wasanii pia kina Izzo B, Adili nk.
Ni tumaini langu kwamba Falsafa ya muziki na maisha kwa Sugu ndio imepelekea kwa kiasi kikubwa kumfanya atumbukie kwenye Siasa na Maisha. Ni dhahiri kwa sasa anawaza Siasa kuliko Muziki. Katika miaka sita ya Ubunge ametoa/kushiriki nyimbo zisizozidi tano wakati kwa miaka sita ya muziki angekuwa ametoa si chini ya album mbili. Baada ya kuwa Mwanamuziki Mkongwe sasa anataka kuwa mwanasiasa mkongwe. Hana budi kusema Kwaheri Muziki na Maisha, Karibu Siasa na Maisha. Kila la kheri Brother Sugu.

No comments:

Post a Comment