Baraza la Sanaa la taifa, BASATA limekuwa
mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa
shughuli za sanaa zinaenda katika mstari
unaotakiwa.
BASATA limedai kumfungia Shilole kutojihusisha
na muziki kwa mwaka mmoja kwa madai ya
kuidhalilisha Tanzania kwa kusambaa picha za
aibu alizopigwa wakati anatumbuiza nchini
Ubelgiji miezi kadhaa iliyopita
Na kwa kiasi kikubwa baraza limekuwa likijitajidi
kuipigania sanaa ya Tanzania kwa namna nyingi
ikiwa ni pamoja na kushiriki katika kuanzisha na
kusimamia tuzo za muziki za Tanzania,
Kilimanjaro Music Awards pamoja na mambo
mengine.
Miongoni mwa masuala mengine ambayo
BASATA imekuwa ikifanya ni kusimamia maadili
kwenye sanaa na kutoa onyo ama adhabu kwa
wanaoyakiuka.
Katika kipindi cha hivi karibuni, BASATA imetoa
adhabu mbili kubwa ambazo ni pamoja na
kuyafungia mashindano ya Miss Tanzania kwa
miaka miwili na adhabu waliyoitoa jana ya
kumfungia Shilole kutojihusisha na masuala ya
muziki kwa kipindi cha mwaka mmoja.
BASATA imetoa adhabu hiyo baada ya miezi
kadhaa iliyopita picha za aibu za Shilole
kusambaa mtandaoni wakati akitumbuiza nchini
Ubelgiji. Kwa mujibu wa Shilole, picha hizo
zilipigwa na mmoja wa watu waliokuwa
wakiangalia show yake na kuzipost kwenye
mitandao ya kijamii. Picha hizo zinaonesha
maziwa ya msanii huyo wazi na kiukweli sio
picha nzuri.
“Nasisitiza tena sikudhamiria na wala sikupenda
hiyo kitu itokee, ila nasikitika kwamba kama mimi
mwanamke yule mtu aliyenipiga picha na
kudhamiria kuziweka kwenye mitandao alikuwa
na maana gani, hakufikiria mimi nitaunmia kiasi
gani au mashabiki wangu wataumia kiasi gani? Ni
mtu mbaya mwenye roho mbaya sijui nimuiteje
huyo mtu aliyefanya hivyo, sio mtu mzuri,” Shilole
alisema kwenye mahojiano aliyofanya.
BASATA walitoa maelezo kueleza namna
walivyosikitishwa na picha hizo na kumuita
Shilole aendee kujieleza. Kwa mujibu wa Shilole,
aliliomba radhi baraza hilo pamoja na mashabiki
wake.
Shilole anaamini kuwa kama aliweza kuomba
radhi zaidi ya mara moja, adhabu hiyo
haikupaswa kutolewa.
Maoni yangu ni kuwa kitendo alichofanya Shilole
kilipaswa kuadhibiwa lakini sio kwa ukubwa huu
wa sasa. Adhabu ya kutojihusisha kwenye muziki
kwa mwaka mmoja kwa muimbaji anayetegemea
muziki na tena mwanamke mwenye familia ni
kubwa mno.
BASATA walipaswa kufikiria kuwa adhabu hii
haitoishia kumuumiza Shilole peke yake, bali hata
familia yake. Shilole ana watoto wawili wa kike
anaowasomesha kupitia muziki. Anasomesha pia
watoto wawili wengine wa ndugu zake.
Na kwa familia zetu nyingi za Kitanzania, ni wazi
kuwa ndugu wengi wa karibu wa Shilole
humtegemea kwa namna moja ama nyingine.
Wategemezi hawa watapata tabu kubwa
kutokana na mama yao kukatiwa chanzo kikuu
kinachomuingizia fedha – shows.
Adhabu hiyo inamaanisha kuwa Shilole atakaa
mwaka mzima bila kufanya show yoyote, ndani
wala nje ya nchi. Kwa mwaka mzima ataishi vipi?
Kwa haraka haraka, BASATA ikishikilia msimamo
wake, Shilole itabidi atafute njia nyingi ya
kujipatia kipato. Ni wazi kuwa huo utakuwa ni
mwanzo wa kumtoa msichana aliyekuwa
amejiajiri kwenye muziki kuingia kwenye shughuli
zisizofaa kama vile kujiuza au kufanya biashara
haramu. Madhara yake baada ya hapo ni
makubwa zaidi.
Adhabu hii ikitimizwa, itamuathiri pia msichana
huyu kisaikolojia na kiukweli athari haziwezi kuwa
ndogo. Wote tunafahamu ukali wa maisha ulivyo
miaka hii na kwa msichana kukatiwa vyanzo
vyake vya kiuchumi kwa mwaka mzika ni adhabu
kubwa mno.
Ninawasihi BASATA kuzingatia athari za adhabu
hii kwa si tu Shilole, bali wanae na watu wengine
wanaomtegemea. Nashauri waipunguze adhabu
hii kwa kumlipisha pengine faini ambayo pia
itakuwa fundisho si tu kwake bali kwa wasanii
wengine.
Ujumbe umeshafika na tena kwa sauti kubwa
kuwa BASATA halitaki kabisa mchezo, lina
mamlaka na kwamba wasanii wanapaswa kuwa
makini kwenye kazi zao kwa kuepuka kutumia
vilevi wanapokuwa jukwaani.
Fundisho ni kuwa wasanii wachukulie muziki
kama ajira zingine kwa kujistahi wao wenyewe na
mashabiki wao. Watambue kuwa nidhamu ya kazi
ni miongoni vitu muhimu vitakavyowasaidia
kutunza heshima za majina yao.
Watambue kuwa matukio kama haya
yatawakosesha fedha nyingi kutoka kwa
makampuni ambayo hayapendi kujihusha na
wasanii wenye sifa mbaya midomoni mwa watu.
No comments:
Post a Comment